RIPOTI: Rais Mugabe kung’atuka madarakani kwa masharti
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amekubali kujiuzulu nafasi ya urais wa nchi hiyo kwa masharti kuwa yeye na mkewe Grace Mugabe wapatiwe kinga ya kudumu na mali zake binafsi zisiharibiwe wakati wa maisha yake yote baada ya kujiuzulu.

Rais Mugabe na mkewe, Grace.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye tovuti ya kituo cha runinga cha CCN zimedai kuwa Rais Mugabe ameshawasilisha masharti hayo kwa njia ya barua na tayari Jeshi la nchi hiyo limekubaliana nayo.
Wakati hayo yakifanyika kwa usiri mkubwa, Chama cha Zanu PF leo kimetangaza kukutana na wabunge, Mawaziri na Maseneta wa Chama hicho mchana huu.
Taarifa hizo zilizovujishwa na watu wa karibu wa Rais Mugabe zimetoka wakati huu ambapo Rais Mugabe alishurutishwa na Chama chake jana jumapili kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya urais wa nchi hiyo.
Hata hivyo bado haijabainika kuwa ni lini kiongozi huyo ataachia madaraka rasmi kwani leo jumatatu saa 6:00 adhuhuri alitakiwa kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo ya urais.
Comments
Post a Comment