Uteuzi wa Dr. W.P.Slaa kuwa Balozi: Rais Magufuli Anaendelea Kujieleza na Kujipambanua Kisiasa
Mwanzo mwanzoni nikiri kuwa nimefarijika sana kwa uteuzi wa Dr. Wilbrod Peter Slaa kuwa Balozi. Uteuzi huo umefanywa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dr. John Pombe Magufuli. Nimefurahi kwakuwa Dr. Slaa, kwa weledi wake, usomi wake, kwa sifa zake uzoefu wake na ubobezi anastahili uteuzi huo au wowote kwa ajili ya kuitumikia nchi. Kwa uteuzi wa Dr. Slaa kuwa Balozi, Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anaendelea kujieleza na kujipambanua. Anajipambanua kuwa anasimamia kauli zake. Mara kwa mara hutamka kuwa 'maendeleo hayana chama'. Na akawahi kukaririwa akisema kuwa anaweza kumteua hata asiye mwanaCCM kama tu ana sifa. Akafanya hivyo kwa Mama Mghwira na kwa Prof. Kitila Mkumbo. Teuzi zake nje ya CCM, pamoja na kwamba zinaweza kuzua malalamiko, manung'uniko na maumivu kwa wanaCCM, zinajieleza na kujipambanua kuwa uwezo, uzalendo na uchapakazi ndiyo vigezo pekee vilivyobaki katika teuzi za Rais Magufuli. Kwake yeye, hakuna tofauti kati ya mwanaCCM au mw...